Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako kuu, na mkono wako ulio hodari, na mkono wako ulionyoshwa; hao watakapokuja na kuomba wakiielekea nyumba hii; 2 Wafalme 6:32.

Wednesday, 13 July 2022

HIJA (PILGRIM)

 UTANGULIZI

1 Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu. Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana, Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana; Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la Bwana. Maana huko viliwekwa viti vya hukumu, Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. Utakieni Yerusalemu amani; Na wafanikiwe wakupendao; Amani na ikae ndani ya kuta zako, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, Amani ikae nawe. Kwa ajili ya nyumba ya Bwana, Mungu wetu, Nikutafutie mema. Zaburi 122:1-9

Hija ni ziara ya kidini yaani ni safari inayofanyika kwa sababu ya dini ikilenga patakatifu fulani. Hujaji na mtalii wanaweza kufuata ratiba hiyo hiyo, lakini hujaji yuko katika safari takatifu ambayo Mungu anakutana naye kupitia mahali, watu na hali.

Mtalii huona vituko, hugundua maeneo mapya, hujifunza mambo ya kuvutia, huchukua picha na kukusanya zawadi. Mtalii anarudi nyumbani mtu sawa na yule aliyeondoka, ila labda kwa akili iliyo na mambo mengi zaidi. Hujaji hupata utambuzi na kutambua ukweli mpya kuhusu yeye mwenyewe. Hujaji husafiri kwa matarajio kuwa mwenye kurejea hatakuwa sawa na yule aliyetoka. Matokeo ya hija yatakuwa ni mabadiliko yaliyotokea ndani ya mtu. Hija atarudi na hisia iliyochapishwa kwenye nafsi, badala ya kumbukumbu ya kamera ya digitali.

Sababu ya kwenda mahali maalumu ni tumaini la kuwa karibu zaidi na imani mahali ambako mambo muhimu ya historia ya dini husika yalitokea; mara nyingi pia imani ya kwamba maombi yatakuwa na nguvu au mafanikio zaidi pale.

Desturi ya kuhiji iko katika dini mbalimbali.

·      Uyahudi tangu zamani unatia maanani hasa hija ya kwenda Yerusalemu, iliyokuwa ya lazima katika sikukuu mbalimbali kwa waumini kuanzia umri wa kubalehee; unaendelea hata baada ya hekalu la mji huo kubomolewa kabisa mwaka 70 BK.                                           

·      Wakristo hasa wa madhehebu ya Kiorthodoksi na Katoliki wanajua hija kwenda Yerusalemu, Roma na mahali pengine.

Kitabu hiki kimelenga kufanikisha hija yako katika Nchi Takatifu ya Israeli pekee kwa kukuonyesha maeneo muhimu ambayo yapo ndani ya maandiko matakatifu. Ni rahisi sanaa kupanga kwenda Israeli kwaajili ya maombi lakini usipojue eneo gani linahusika na aina ipi ya maombi unaweza kurudi bila kile ulichotarajia. 

Roho Mtakatifu amefunua siri zake kwetu ili tuweze kufanikisha hija yako na kuwa na matokeo chanya kwenye maombi yako kwa ujumla. Mara nyingi wanaotuongoza (guide) kwenye safari hizi za Nchi takatifu wanatupa historia ambayo ukichunguza kwa makini ni kitu walichosomea kwa miaka mingi, na hakina mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako ya kiroho. 

Unaweza kujiuliza swala kwamba hii inakuwaje kusema ni historia tu?

Tuangalie kidogo kwenye maandiko Matakatifu ambayo ndiyo kiongozi wetu kama waamini wa Kristo. 

Matendo Ya Mitume 8:27-40

27 Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, 28 akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. 29 Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. 30 Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? 31 Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. 32 Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. 33 Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. 34 Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? 35 Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. 36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? 37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] 38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. 39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi. 40 Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.

Alipokuwa anaenda kuabudu kwa lugha ya kawaida alikuwa anaenda kushiriki ibada, kwa tafsiri ya kuabudu au kwa lugha ya sasa ambayo wengi tunafahamu tungesema amekwenda hija.  

Huyu mtu ameshuka kwenda Yerusalemu kutoka Kushi ambayo ni Ethiopia kwa sasa. Kutoka Ethiopia mpaka Israeli ni kama miles 1,550. Kwa vyovyote alitumia gharama kwaajili ya matayarisho ya safari yake na alijua umuhimu wa kwenda Yerusalemu kuomba. Nataka uone kwamba hizi safari za kwenda mahali kwaajili ya kuutafuta uso wa Bwana hazikuanza katika kipindi cha karne ya sasa ni miaka mingi iliyopita. 

Huyu mtu ameenda ibadani hajaokoka hajamjua Mungu, lakini ndani yake anatafuta kumjua Mungu sio kanisa. Biblia inaita kuabudu hatafuti kulijua kanisa bali kumjua huyo Mungu, alietengeneza ile madhabahu ikawepo na watu wanajikusanya wanasema wanaenda kuabudu. Madhabahu maana yake ni mahali ambapo watu wameweka mahusiano na Mungu wao na wametengeneza mahali pa kukutana nae huyo Mungu wao. Sasa huyu ndugu ametoka kwenye ibada hajaona alichokuwa anatafuta, kwa sababu hajaenda kusali tu kama kusali, alienda kutafuta mahusiano yake na Mungu. Na Biblia inasema yeyote amtafutaye kwa bidii atamuona haijalishi ni wa kabila na dini gani ndani yake kama ana kiu Mungu hataficha uso wake kuna namna ambavyo atajifunua kwake.

Nataka kukueleza juu ya umuhimu wa kufanya hija yenye nguvu za Mungu si swala la kusafiri na kwenda Nchi takatifu tu. Maandiko yanasema wazi kwamba “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamuMathayo 15:8-9. Nataka uone lile neno linasema nao waniabudu bure”unaweza kwenda Israeli na ikawa bure pasipokuwa na muongozo sahihi wa kitu gani chakufanya. Madhumuni makubwa ya kitabu hiki ni kuhakikisha kwamba unakwenda na kupata kila ambacho Mungu amekusudia kwa kila mmoja anayekwenda na kuutafuta uso wake. 

Nimeona watu wengi sana wakipinga swala hili la kwenda Israeli na wengine wakisema hakuna umuhimu kabisa na wananukuu maandiko kabisa. Unajua katika hali ya Imani ni muhimu kuwa makini kwamba unamsikia nani na anaongozwa na nani? Siyo kila jambo watu wote wanafunuliwa na ndiyo maana Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.Zaburi 25:14.Kinachokuza Imani yako ni namna unavyolicha jina la Bwana na namna unavyotetemeka mbele zake na kumuelewa yeye kupitia neno lake si kwenda Israeli pekee. Jaribu kufikiri safari ya siku tano kila siku tunaongelea Biblia tu pekee bila kuchanganya na mambo mengine mengi simu za nyumbani na mambo ya kazini kwako lazima kuna neno litaingia ndani yako. Nasi tunatenga siku hizi za hija maalumu kwaajili ya kuomba na kutafakari ukuu wa Mungu tukiwa maeneo ambayo Biblia iliandikwa huko. 

Huyu ndugu alikwenda Hekaluni akiwa na kiu ya kumuona Mungu aliyeziumba mbingu na Nchi na akiamini kabisa kama vile kitabu cha 2 Nyakati 7:14kinavyosema “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.Kwa hivyo alikuwa na uwakika wa kusema na Mungu lakini maandiko yanasema alikuwa anarudi kwao Ethiopia bila kujua kitu au kupata kile alitarajia kupata kweye ibada yake. 

Ni rahisi sana kusoma habari za huyu ndugu na usijue kile kiliendelea na kiu iliyokuwa ndani yake hata kupelekea Filipo aliyekuwa kwenye uamsho mkubwa wa injili huko Samaria kuambiwa aende kwa huyu ndugu. Sasa kile kilichovuta nguvu za Mungu ni aina ya kiu aliyekuwa nayo huyu ndugu ndipo Bwana akajibu na kumtuma Filipo. 

Bwana ametupa nafasi hii ili kuweka kiu ndani yako ili kabla haujafika Nchi takatifu ujue ni namna gani ya kuomba katika maeneo tofauti tofauti. Kila eneo linakusudi lake na yapo mambo mengi sana yametendeka kwa kila eneo. 

Israeli ni Nchi ambayo imejaa vitu vingi sana ambavyo kiuhalisia kila kimoja ni cha kiimani inategemeana na namna unavyoona maandiko yanasema “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe” Mithali 23:7. Namna unavyoona kila kitu ndivyo itakavyokuwa kwako ukiona umekwenda kwa misingi ya utalii utapata hicho hicho. Lakini ukienda kwaajili ya hija hakika utapata vile unavyotaka katika hija yako. Tumeweka kitabu hiki kwenye mikono yako kwa kusudi la kukuongoza kwa kila eneo la hija yako ili ufurahie na kupata matokeo mazuri kwenye maisha yako hapa Duniani. 

Kuna mambo ya kihistoria ambayo kimsingi utayapata sana ukiwa Nchini Israeli lakini kwenye kitabu hiki nikuhakikishie tu kwamba tutakutazamisha yale ambayo ni ya Rohoni kwaajili ya msaada wa hija yako. Kumbuka jambo hili kila mara hija ni safari ya kiroho kwaajili ya mahali fulani Patakatifu. Najua kabisa watu wengi wamekwenda katika Nchi takatifu na wengine wamerudi wakiwa na tumaini jipya na wengine wamerudi katika hali ya kawaida kabisa ni matumaini yangu kwamba safari yako haitakuwa yakawaida katika maisha yako. Tumekuandalia kitabu hiki ili kikuwezeshe na kukuongoza katika hija yako na kukupa mwanga wa kiroho. Kitabu hiki kimejaa mambo ambayo mengi sana utakutana nayo maeneo husika lakini ni kiongozi kwaajili ya maswali yako ambayo unaweza kuwa nayo katika kipindi chote cha safari yako. 

Safari hizi ni ibada katika maisha yako, na tunatumaini katika utumishi huu utafurahia na kusonga mbele kwenye maisha yako. 

Kitabu hiki tumekigawa katika sehemu kuu mbili sehemu ya kwanza inahusiana na historia ya kawaida ya maeneo muhimu ya Israeli, na maeneo mengine kama Misri na Yordani sehemu ya pili inahusiana na muongozo wa kimaombi wa kila eneo ambalo ni la kihistoria kulingana na maandiko matakatifu. 

Katika Safari yako ni muhimu kwenda na kanuni hizi:

      I.        Kabla ya hapo, tarajia kile utakachoona kwa kusoma kukihusu.

    II.        Unapofika hapo, karibia eneo kwa matarajio yote unayoweza kupata, kana             kwamba ni sehemu pekee duniani ambayo ni muhimu.

  III.        Unapofika, tambua uwepo wake Mtakatifu, ukichukua muda kuwa peke yako, wewe mwenyewe na Mungu.

 IV.        Baada ya kuondoka, andika mawazo yako ya baadae kuhusu yale uliyopitia.

Karibu kwenye safari yenye nguvu za Mungu kwenye maisha yako. 

Mungu akubariki sana. 

Pastor Daniel Lema. 

No comments: